Na Muandishi Wetu.
Wakuu wa Mamlaka za Kodi kutoka Jumuiya za Afrika Mashariki na Afrika Magharibi wakiongozwa na uwakilishi kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) wameipongeza Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) kutokana na hatua inazopiga katika mageuzi ya matumizi ya mifumo ya ukusanyaji kodi.
Viongozi hao ambao wapo nchini kwa mkutano wa wiki moja unaotathmini matumizi ya Teknolojia katika Utoaji wa huduma bora na ukusanyaji kodi, walitoa pongezi hizo leo walipotembelea Afisi za ZRA Mazizini ikiwa ni kwa lengo la kujionea namna taasisi hiyo ilivyopiga hatua katika matumizi ya teknolojia katika kuimarisha huduma za kodi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Muwakilishi wa IMF ndugu Henry Gaperi alisema ziara hiyo imeshuhudia Zanzibar kuwepo kwa vijana wenye vipaji na uwezo mkubwa katika utengenezaji wa mifumo, na akaipongeza ZRA kwa kutengeneza mifumo ya kodi kwa kutumia wataalamu wa ndani.
Aidha, bwana Henry aliongeza kuwa, ni vyema ZRA ikawa na mikakati imara ya kutumia mifumo hiyo inayotengenezwa na wataalamu wake ili iweze kusaidia katika ukusanyaji wa mapato kwa maslahi ya Taifa.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Liberia (LRA) ndugu Thomas Gunnar alisema walichokishuhudia Zanzibar si jambo la Kawaida na kwamba ujumbe huo umejifunza mengi ambayo wanapaswa kuyaiga kwa mafanikio ya ukusanyaji kodi katika nchi zao.
Naye Kamishna Mkuu wa ZRA ndugu Yusuph Juma Mwenda alisema ZRA imefarajika kwa kupokea ugeni huo kwani imeweza kubadilishana uzoefu na mataifa mbali mbali katika matumizi ya Teknolojia na ukusanyaji kodi.
Pamoja na kutembelea Makao makuu ya ZRA Mazizini, Viongozi hao wa Mamlaka za Kodi Afrika Mashariki na Afrika Magharibi walipata nafasi ya kutembelea Vituo vya mafuta pamoja na Hoteli kadhaa ili kujionea namna mfumo wa kutolea Risiti za Kielektroniki unavyofanya kazi.
Jumla ya mataifa kumi na tatu (13) yalishiriki katika ziara hii yakiwemo mataifa ya Uganda, Kenya, Rwanda, Ghana, Ethiopia, Cape Verde, South Sudan na Liberia.