BODI ya Mapato Zanzibar (ZRB), inakusudia kukaa pamoja na Tasisi za Serikali ambazo zina mchango katika ukusanyaji wa mapato ikiwemo Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na Bandari ili kuhakikisha inaondoa changamoto na kuongeza kasi ya ukusanyaji.
Hayo yalielezwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Saleh Sadiq Osman, wakati akizungumza na Zanzibar leo mara baada ya kumaliza ziara iliyowashirikisha watendaji mbalimbali wa Bodi hiyo walipotembelea Uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume, Bandari ya Malindi na Bohari kuu ya Mafuta Mtoni.
Alisema, ikiwa Taasisi hizo zitaweza kukaa pamoja na kushirikiana kwa kila jambo basi wataweza kutatua changamoto zinazowakabili na kuongeza mapato yanayotegemewa na Serikali katika shughuli za kimaendeleo.
Aidha, alisema kuna changamoto kadhaa ambazo zimeonekana katika ziara hiyo hivyo watahakikisha wanazifanyia kazi ili kuona kiwango cha ukusanyaji wa kodi kinachotakiwa na serikali kwa mwaka 2017/2018 kinafikiwa kama ilivyokusudiwa.
Mwenyekiti huyo alibainisha kuwa, kwa kuwa ZRB ni chombo kilichopewa dhamana ya uwakala ya ukusanyaji wa kodi za ndani kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ni wajibu wao kutafuta uwezekano wa kila pahali kwa mujibu wa sheria kuweza kukusanya kodi na kuweza kuingiza katika mfuko mkuu wa Serikali.
"Dhamana tuliyopewa ni jukumu letu kuhakikisha tunaisimamia vyema tena kwa nguvu zote ili kusudi Serikali iweze kutumia fedha hizi kwa kuleta maendeleo nchini," alisema.
Hata hivyo, akizungumzia lengo la ziara hiyo alisema imetokana na makubaliano ya Bodi kuona sehemu zinazowahusu katika ukusanyaji wa mapato ikiwemo tasisi hizo na kuona mapato ya serikali hayapotei kiholela.
"Madhumuni makubwa ni kuona vipi tutaweza kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa mapato ili kusaidia katika uendeshaji wa shughuli za kimaendeleo nchini," alisisitiza.
Katika hatua nyengine, aliwasisitiza watendaji ambao wamepewa jukumu la ukusanyaji wa kodi katika tasisi hizo kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao ipasavyo na lengo lilokusudiwa linafikiwa kwa kiwango kikubwa.
Nao, baadhi ya wafanyakazi walisema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutopata Ankara sahihi za kodi kwa wafanyabiashara.
Changamoto nyengine, walisema ni kuondoka kwa wafanyabiashara wadogo wadogo kunapotokana na kutozwa kodi mara mbili hali ambayo inapelekea kupunguza kwa mapato kutoka katika eneo hilo.
Katika hatua nyengine, walisema changamoto kubwa katika suala la mafuta ni uletaji wa mafuta nchini kwa kuchelewa ambao unaweza kuleta taharuki kwa wananchi hasa watumiaji wa bidhaa hiyo na kutofikia malengo ya Bodi hiyo katika ukusanyaji wa mapato yake.