Mwenda kuwa Kamishna Mkuu wa kwanza
Na Muandishi Wetu.
Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Fedha na Mipango Mheeshimiwa Dkt. Saada Mkuya Salum ametangaza rasmi kuanza kutumika kwa jina la Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) badala ya jina la Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) ambalo lilikuwa likitumika zamani kuitambulisha taasisi hiyo.
Waziri Saada amefanya uzinduzi huo leo katika mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika katika ukumbi wa ZRA Mazizini na kuongeza kuwa uzinduzi huo umefanyika baada ya kusainiwa kwa Sheria hiyo na hatimaye kutangazwa rasmi katika Gazeti la Serikali.
Dkt. Saada amesema kuwa ujio wa ZRA hauna lengo wala dhamira ya kuongeza viwango vya kodi kwa wafanyabiashara, bali ni kwa kuleta mabadiliko katika utendaji sambamba na kutoa huduma zenye viwango vya kimataifa pamoja na kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato nchini.
Ameongeza kuwa, ZRA imekuja kufuta mitazamo hasi ambayo ilidumu kwa muda mrefu kwa jamii juu ya Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), hivyo aliwaomba walipakodi na wananchi kwa ujumla kuwa na imani na Taasisi hiyo ambayo imejipanga kukusanya kodi na kuwasimamia wanaostahiki kulipa kodi ili kwa pamoja kuinua mapato ya nchi.
Wakati huo huo Dkt Saada ameutangazia umma kuwa kutokana na kuridhishwa na utendaji mzuri katika suala la ukusanyaji wa mapato, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi amemteua Ndg. Yusuph Juma Mwenda kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka Mapato Zanzibar (ZRA).
Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa ZRA Ndg. Yusuph Juma Mwenda amesema kuwa ZRA haitatumia nguvu katika ukusanyaji wa mapato, itarahisisha miundombinu ya ukusanyaji kodi kwa kuwaweka karibu walipakodi.
Aidha, Kamishna Mwenda amesisitiza kuwa katika kipindi hiki cha mpito nyaraka zote pamoja na nembo zilizokuwa zikitumiwa na ZRB zitatambulika kuwa ni nyaraka halali kwa ZRA mpaka pale taarifa nyengine rasmi zitakapotolewa.
Jee Wajua
Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) imebadilishwa jina, na sasa itatambulika kwa jina la Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA).
Fahamu
Hakuna mabadiliko yoyote wala ongezeko la Kodi litakalotokea kwa Walipakodi kutokana na kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA).
Habari Ikufikie Kuwa…
Nembo na Nyaraka nyengine zilizokuwa za Bodi ya mapato Zanzibar (ZRB) zitaendelea kutumiwa na Mamlaka ya mapato Zanzibar (ZRA) hadi hapo itakapotangazwa vyenginevyo.