Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) imesema magendo ya mafuta na uuzaji wa nishati hiyo kwenye madumu katika vituo vya kuuzia mafuta (sheli), ni moja ya changamoto kubwa inayoendelea kuitesa kwa muda mrefu sasa.Hayo yalisemwa na wajumbe wa bodi hiyo walipofanya ziara katika vituo mbali mbali vya kuuzia mafuta kisiwani hapa na kujionea nishati hiyo ikiuzwa kwenye madumu, hali ambayo inasababisha serikali kukosa mapato yake.
Walisema wakati umefika kwa ZRB kuchukua hatua za kisheria ili kukabiliana na tatizo hilo ambalo limeshamiri maeneo mbali mbali Unguja na Pemba.
Uuzaji wa mafuta kwenye madumu na kwa njia ya magendo ni maarufu katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar ikiwemo Mikunguni Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja ambapo biashara hiyo inafanywa bila kificho.
Akizungumza na Meneja wa kituo cha kuhifadhia mafuta cha kampuni ya Gapco, Wesha, Mwenyekiti wa Bodi ya ZRB, Saleh Saidik, alimtaka Meneja huyo kushirikiana na ZRB katika kukusanya mapato, ili serikali iweze kupata stahiki yake.
Alisema kampuni hiyo inapaswa kushirikiana na ZRB kuwakamata watu wanaoingiza mafuta kwa njia ya magendo kwani wanasababisha serikali kushindwa kukusanya mapato.
Aidha aliitaka ZRB ofisi ya Pemba, kufanya msako katika vituo vyote vinavyouza mafuta na kuwachukulia hatua wanauza mafuta kwenye madumu.
Kamishana wa ZRB, Amour Hamil Bakar, alisema mikakati madhubuti inaandaliwa kwa ajili ya kuwachukulia hatua wale wote wanaouza mafuta kwa njia ya madumu.
Meneja wa Gapco katika kituo kikuu cha mafuta Wesha, Justice Mkubi, alisema kazi yake kubwa ni kupokea mafuta na kuyauza kwa jumla na rejareja.
Alisema kwa mwezi alikuwa nauza lita milioni moja za mafuta za petrol lakini kwa sasa anauza lita 500,000.