SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesema inakusudia kuanzisha sheria ya ushuru wa bidhaa ili kuiwezesha Zanzibar kuwa na nguvu za kisheria kutoza ushuru huo. Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Khalid Salum Mohammed, katika mafunzo kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi juu ya rasimu ya sheria ya ushuru wa stempu.
Alisema ZRB imekuwa ikukusanya ushuru kwa huduma zinazotolewa Zanzibar zikiwemo za benki na mawasiliano bila ya kuwa na nguvu za kisheria.
Hivyo alisema kuanzishwa kwa sheria hiyo itaifanya ZRB kuwa na nguvu ya kisheria na kusaidia kuongezeka mapato ya ndani.
Alisema kwa muda mrefu sheria hiyo imekosekana na hivyo kutozwa ushuru wa bidhaa kwa kutumia sheria ya muungano jambo lililosababisha usumbufu kwa wafanyabiashara.
Alisema mbali na sheria hiyo pia serikali itaifuta sheria ya ushuru wa stempu nambari 6 ya mwaka 1996 na kutunga sheria mpya ili kuwaondoshea usumbufu wafanyabiashara wadogo wa kulipa kodi katika taasisi mbili; ZRB na TRA.
Akiwasilisha mada kuhusu uanzishwaji wa matumizi ya mashine za kielektroniki za EFDs, Meneje Sera, Mipango na Utafiti wa ZRB, Ahmed Haji Saadat, alisema kuwepo kwa kifaa hicho kitasaidia kudhibiti na kusimamia uwekaji kumbukumbu na uchunguzi wa bidhaa na mauzo kwa mujibu wa masharti ya sheria.